FEBRUARI 18, 2020; JUMANNE: JUMA LA 6 LA MWAKA

Mt. Teotoni, Abati;
Kijani,
Zaburi: Juma 2.

SOMO 1: Yak. 1: 12-18
Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo, asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu;” maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 94: 12-15,18-19

 1. Ee Bwana, heri mtu Yule amwadibuye na kumfundisha,
  kwa sheria yako;
  Upata kumstarehesha siku ya mabaya.
  (K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.
 2. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake,
  Wala hutauacha urithi wake,
  Maana hukumu itarejea haki,
  Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)
 3. Niliposema, mguu wangu unateleza;
  Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
  Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,
  Faraja zako zaifurahisha roho yangu. (K)

INJILI: Mk. 8: 14-21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, “Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, “Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande?” Wakamwambia, “Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande?” Wakamwambia, “Saba.” Akawaambia, “Hamjafahamu bado?”

TAFAKARI:
KUSAHAU MUDA MWINGINE HUTURUDISHA NYUMA KIIMANI:
Mungu ametutendea mambo mema mengi sana katika maisha yetu. Kila mmoja wetu anaweza kuwa shuhuda wa maisha yake mwenyewe na kila mtu anafahamu ni vitu vingapi Mungu amemtendea katika maisha yake. Jambo la kwanza ambalo Mungu ametujalia ni zawadi ya uhai. Katika Injili, wanafunzi wa Yesu wamesahau kuchukua mikate na pia wamesahau kuwa Yesu aliwalisha watu wengi mikate michache tu, Yesu anawakumbusha. Hata sisi wenyewe huwa tunasahau mambo mengi tuliyotendewa na Mungu hasa tuwapo katika majaribu na mahangaiko, muda mwingine kuhisi Mungu ametuacha na kutusahau. Basi tuwapo katika majaribu tusiseme Mungu anatujaribu, bali ni sisi wenyewe tunaojiingiza katika majaribu hayo kwa tamaa zetu mbaya kama anavyotuambia Mtume Yakobo. Tusiwe na mioyo mizito ya kuamini, na tukitenda dhambi ambazo hupelekea mauti tufanye toba na kujipatanisha na Mungu kwani yeye anatupenda na hawezi kutuacha wala kutujaribu.

SALA: Kwa msaada wako Bwana, twakuomba utujalie tuushinde ugumu wa mioyo yetu.