FEBRUARI 17, 2020; JUMATATU: JUMA LA 6 LA MWAKA

Wat. Waanzilishi Saba wa Shirika la Bikira Maria
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Yak .1: 1-11
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu. Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno. Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husitasita katika njia zake zote. Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa; bali tajiri kwa kuwa ameshushwa, kwa maana kama ua la majani atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea: Vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119:67, 68, 71, 72, 75, 76

  1. Kabla sijateswa mimi nalipotea,
    Lakini sasa nimelitii neno lako.
    Wewe U mwema na mtenda mema,
    Unifundishe amri zako.
    (K) Rehema zako, Ee Bwana,
    zinijie nipate kuishi.
  2. Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
    Nipate kujifunza amri zako.
    Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
    Kuliko maelfu ya dhabihu na fedha. (K)
  3. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
    Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
    Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
    Sawa sawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. (K)

INJILI: Mk. 8: 11-13
Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, “Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni: Hakitapewa ishara kizazi hiki.” Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.

TAFAKARI:
TUSIMJARIBU MUNGU WETU:
Kujaribu ni kupima ili uone nini kitatokea. Tukiamua kumfuata Kristo, tuwe kweli wafuasi wake wa dhati na wala si wale wanaotaka kumjaribu kama walivyofanya Mafarisayo katika Injili. Tukiwa na imani thabiti kwa Mungu isiyokuwa na mashaka kama Mtume Yakobo anavyotuelekeza katika somo la kwanza, tutapata kila kitu tuombacho kwake kama kitakuwa cha manufaa kwetu na cha kumtukuza Mungu. Tukiwa na imani yenye mashaka tusitegemee kitu kutoka kwa Mungu. Pia sisi wenyewe tujaribiwapo tusikate tamaa kwani majaribu mwishowe huleta saburi. Tudumu katika imani yetu, tuwapo na maelekeo ya kuiacha njia ya Bwana. Tutubu na tuombe neema yake ili tuweze kurudi katika njia yake. Tutakutana na tunaendelea kukutana na watu wenye kutukatisha tamaa. Mara utasikia, “nyie mmepotea, njoo huku ndiko kuna Mungu wa kweli.” Mafundisho tofauti tofauti tunayoyasikia katika wakati wetu yasiyo ya imani yetu yasiwe chanzo cha kuiacha imani yetu au kuwa na shaka nayo.

SALA: Ee Bwana, tujalie imani isiyokuwa na mashaka na majaribu yatupatayo yasitukatishe tamaa.