Wt. Sirili, Mtawa, na Metodi Askofu,
Kumbukumbu,
Kijani,
Zaburi: Juma 1.
SOMO 1: 1 Fal. 11: 29-32; 12: 19
Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, “Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, ‘Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi; lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu, mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli.’” Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 81:9-14
- Usiwe na Mungu mgeni ndani yako
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana Mungu wako
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri.
(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako:
Lisikieni sauti yangu. - Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
Waenende katika mashauri yao. (K) - Laity watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Ningewadhili adui zao wa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu. (K)
INJILI: Mk. 7: 31-37
Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, “Efatha,” maana yake, “Funguka!” Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, “Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.”
TAFAKARI:
NI WAJIBU WETU KUHUBIRI INJILI: Leo tunafanya kumbukumbu la Watakatifu Sirili na Metodi ambao baada ya kupewa upadre walienda kuhubiri Injili katika nchi ya Moravia. Walifanya bidii ya kuihubiri imani ya Kikristo bila kujali changamoto na magumu waliyokumbana nayo katika kazi hiyo njema. katika Injili, wazo la kuhubiri Injili linaendelea hasa pale tunapomuona Bwana Yesu akiwa katika mipaka ya Dekapoli anamponya mtu aliyekuwa kiziwi, licha ya kuwaambia watu wasimwambie mtu yeyote juu ya yaliyotendeka, wao wanazidi kueneza na kutangaza habari za mambo makubwa na ya kushangaza aliyofanya Bwana Yesu. Na hivi, Habari Njema juu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu dhaifu inaenea haraka na watu wanatatuliwa shida zao. Nasi kama wakristo tukiiga mfano wa watakatifu wa leo, tunawajibu wa kuhubiri Injili katika mazingira yetu kwa maneno na matendo yetu bila kujali changamoto na magumu tunayoweza kukutana nayo kwani Bwana Yesu alituagiza akisema ‘enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe mkiwafanya kuwa wanafunzi wangu’ (Mk 16:15).
SALA: Ee Bwana, utufanye wahubiri wazuri wa Neno lako kwa wenzetu kwa maneno na matendo yetu.