FEBRUARI 10, 2020. JUMATATU: JUMA LA 5 LA MWAKA

Mt. Skolastika, Bikira,
Kumbukumbu,
Kijani,
Zaburi: Juma 1.

SOMO 1: 1 Fal. 8: 1-7, 9-13
Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli walikutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng’ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana. Ndipo Sulemani akanena, “Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 132: 6-10

 1. Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,
  katika konde Yearimu tuliiona.
  Na tuingie katika maskani yake,
  tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake
  (K) Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako.
 2. Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako,
  Wewe na sanduku la nguvu zako.
  Makuhani wako na wavikwe haki,
  watauwa wako na washangilie.
  Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
  usiurudishe nyuma uso wa masihi wako.(K)

INJILI: Mk. 6: 53-56
Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genezareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

TAFAKARI:
KIMBILIO LA KWELI LA SHIDA ZETU NI MUNGU:
Wapendwa katika Kristo, tuwapo na shida tumkimbilie Mungu naye atatusaidia kwani wote waliomkimbilia na kumuomba kwa imani hakuwaacha. Mfano mzuri unaoneshwa na Mtakatifu Scholastika tunayemkumbuka leo. Yeye alipokuwa bado na hitaji la kusikiliza mafundisho kutoka kwa kaka yake Mtakatifu Benedikto aliyekuwa anaondoka, alimuomba Mungu ili kaka yake asiondoke na kweli alisikia kilio chake na kuleta mvua kubwa yenye radi na kaka yake hakuondoka. Pia katika Injili wote waliomkimbilia Yesu kwa imani walipona, kwani kwa kugusa tu pindo la vazi lake, wote waliokuwa hawajiwezi walipona. Tukiwa na shida ziwe za kifamilia, kiafya, kiimani na kadhalika, tusikate tamaa bali tumwamini Mungu na kumkimbilia naye atatusaidia kwani anatupenda na upendo wake kwetu hauna kifani. Daima Mungu awe kimbilio letu la kwanza tunapopatwa na shida na hii inawezekana endapo tutakuwa na uhusiano mwema naye kwa kuzishika amri zake na kuziishi.

SALA: Baba wa mbinguni, tunakuja kwako tukiwa na matatizo na mahitaji mbalimbali, tunakuomba utupokee na ututimizie kadiri ya mapenzi yako.