FEBRUARI 9, 2020. JUMAPILI: JUMA LA 5 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa. 58: 7-10
Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, “Mimi hapa!” Kama ukiiondoa nira, isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa, ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani, na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 112: 4-9

 1. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
  Ana fadhili na huruma na haki.
  Heri atendaye fadhili na kukopesha;
  Atengenezaye mambo yake kwa haki.
  (K) Nuru huwazukia wenye adili gizani.
 2. Kwa maana hataondoshwa kamwe;
  Mwenye haki atakumbukwa milele.
  Hataogopa habari mbaya;
  Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana. (K)
 3. Moyo wake umethibitika hataogopa,
  Hata awaone watesi wake wameshindwa.
  Amekirimu, na kuwapa maskini,
  Haki yake yakaa milele,
  Pembe yake itatukuzwa kwa utukfu. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 2: 1-5
Ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno,wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lo lote ila Yesu Kristu, naye amesulibiwa. Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukua kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.

SHANGILIO: Mdo. 16:14
Aleluya, aleluya,
Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, Mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.
Aleluya.

INJILI: Mt. 5: 13-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

TAFAKARI:
KUTOA NI TIBA VIDONDA VYA MOYONI NA MSONGO WA MAWAZO:
Ukweli huo unabainishwa na somo la kwanza. “Uwagawie wenye njaa mkate wako…ndipo mwanga wako utatokea kama alfajiri, na vidonda vyako vitapona upesi” (Isaya 58: 7-8). Hadithi ifuatayo inabainisha ukweli huu. Maisha ya John D. Rockfeller wa Marekani yanabainisha ukweli huo. Akiwa na umri wa miaka thelathini na tatu alikuwa tayari amejipatia dola milioni moja, kadiri ya Dale Carnegie katika kitabu chake- How to Stop Worrying and Start Living. Akiwa na umri wa miaka 43 alikuwa na Kampuni kubwa ya mafuta -Standard Oil Company. Alipokuwa na miaka 53 alikuwa wapi? Alidhoofishwa na hofu.Alipatwa na ugonjwa uliofyeka nywele zake. Alilazimishwa kuishi kwa kunywa maziwa kidogo. Katika umri huo alionekana mzee sana sababu ya hofu isiyo na kikomo. Alikuwa tajiri sana duniani lakini aliishi kwa mlo ambao hata maskini angedharau kuuchukua. Matibabu ya hali ya juu yalichelewesha kifo chake.
Alipopata faida alicheza dansi ya kivita na alipopata hasara alikuwa kama mgonjwa, alienda kitandani kulala. Mambo yaliyomdhoofisha yalikuwa hofu, uchoyo na wasiwasi. Baadaye madaktari walimshauri kutokuwa na hofu, kupumzika, kuwa makini na anachokula na kufanya mazoezi. Lakini alifanya jambo la zaidi. Aliacha kufikiria sana kiasi cha pesa cha kupata na kuanza kufikiria kiasi cha pesa cha kutoa na kusaidia watu. Alitoa mamilioni ya hela. Alianzisha taasisi iliyoitwa Rockfeller Foundation ambayo ilipigana dhidi ya maradhi na ujinga duniani kote. Alisaidia tafiti mbalimbali zilizopelekea kwenye vumbuzi mbalimbali kama muujiza wa penicillin. Baada ya kuanza kutoa alibadilika kabisa. Alipata amani ya moyoni. Ingawa alichungulia kaburi akiwa na umri wa miaka 53 baada ya kubadili mtazamo na kuanza kutoa aliishi na kufikia umri wa miaka 98.
Kutoa ni sababu ya mafanikio. Mtu anaweza kufilisika si kwa sababu anatoa bali kwa sababu hatoi. Asiyepoteza haokoti. Kwamba kutoa ni sababu ya mafanikio, jambo hili limethibitishwa na watu wengi. “Mtu mwenye busara haweki hazina kwa ajili yake. Anavyotoa zaidi kwa wengine, ndivyo anapata zaidi sana,” alisema Lao-tzu. Mawazo hayo yanafanana na ya Anne Sophie Swetchine aliyesema: “Tuko matajiri kupitia tu tunachokitoa.” Ukweli ni kuwa tunazidisha kwa kugawana. Leonard Nimoy alisema, “Muujiza ni huu: tunavyogawana zaidi tunakuwa na zaidi.” “Binadamu ni kama shimo: kadiri unavyochukua zaidi kutoka kwake ndivyo anavyopata kuwa mkubwa. Ukubwa upo katika msingi wa kutoa, si kupata,” alisema Richard C. Jalverson.


SALA: Ee Mungu nisaidie moyo wangu ujae ukarimu niweze kutoa na kusaidie wengine. Amina.