FEBRUARI 8, 2020. JUMAMOSI: JUMA LA 4 LA MWAKA

Mt. Hieronimo Emiliano
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: 1 Fal. 3: 4-13
Mfalme Sulemani alienda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, “Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119: 9-14

 1. Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?
  Kwa kutii akilifuata neno lako.
  Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
  usiniache nipotee mbani na maagizo yako.
  (K) Unifundishe amri zako, Ee Bwana.
 2. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
  nisije nikakutenda dhambi.
  Ee Bwana umehimidiwa, u
  nifundishe amri zako. (K)
 3. Kwa midomo yangu nimezisimulia
  hukumu zote za kinywa chako.
  Nimefurahi njia ya shuhuda zako
  kana kwamba ni mali mengi. (K)

INJILI: Mk. 6:30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, “Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo.” Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.

TAFAKARI:
TUJALI MAHITAJI YA WENZETU:
Kwa kawaida, baada ya kazi huwa tunapumzika na muda mwingine kupata chakula na kinywaji ili kujipatia nguvu mpya ya kuendelea na kazi wakati mwingine. Katika Injili, tunamwona Bwana Yesu akitambua hitaji la mitume wake baada ya kupewa mrejesho wa kile walichokifanya, na hivi wanatafuta sehemu ya faragha mashuani ili wapate kuvuka ng’ambo ya pili kusiko watu ili wapate kula na kupumzika. Na aliposhuka mashuani, kwa kutambua hitaji la mkutano mkuu akawahurumia na kuanza kuwafundisha mambo mengi. Mfalme Sulemani kwa kutambua mahitaji ya watu wake aliomba hekima ya kuwahukumu vema. Kama wakristo, tuna watu mbalimbali wanaotuzunguka katika sehemu zetu tunazoishi, ni wajibu wetu kuwa na jicho la utambuzi ili tuweze kuwasaidia wahitaji kama wagonjwa, maskini, yatima na wazee, tukiiga mfano wa Mtakatifu Hieronimo Emiliano aliyetimiza wajibu huo kwa maombezi ya Bikira Maria.

SALA: Ee Bwana, tujalie neema ya kuwa msaada kwa wahitaji katika jamii zetu.