Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mal. 3:1-4
Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo: naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 24:7-10
- Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu?
Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari. - Ni nani Mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu, hodari,
Bwana hodari wa vita. (K) - Inueni vichwa vyenu, enyi milango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K) - Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye Mfalme wa utukufu. (K)
SOMO 2: Ebr. 2:14-18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
SHANGILIO: Lk. 2:32
Aleluya, aleluya
Nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa,
na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
Aleluya.
INJILI: Lk. 2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana, wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.” Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
“Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake” (Lk 2: 26-27).
TAFAKARI:
WEKA MKAZO KWENYE HEKALU AU KANISA: Injili inaweka mkazo kwenye hekalu. Ufunuo unaotutayarisha kwa ajili ya maisha ya Yesu unatokea Yerusalemu hekaluni. Hekalu la Yerusalemu ni mahali ambapo hatima ya Yesu inajifungua mwishoni mwa safari yake. Yerusalemu ni mji wa mateso na kutukuzwa kwa Yesu. Kwa wafuasi hekalu la Yerusalemu ni mahali walipokuja tena baada ya Yesu kupaa mbinguni.
“Kutolewa Yesu hekaluni kunamwonyesha kama mzaliwa wa kwanza ambaye ni wa Bwana. Pamoja na Simeoni na Anna, Israeli yote inangoja kukutana na Mwokozi wao. Yesu anatambuliwa kama Masiha aliyengojewa, ‘Nuru ya mataifa’ na utukufu wa Israeli, lakini pia ishara itakayonenewa. Upanga wa uchungu aliotabiri wa Maria, unatangaza sadaka nyingine kamilifu na ya pekee ya msalaba itakayoleta wokovu ambao Mungu ameutayarisha mbele ya macho ya watu wote” (KKK Na 529).
Upanga wa uchungu wa Bikira Maria unatufundisha matatizo si alama ya kusimama ni alama ya kupia. Bikira Maria alipoambiwa uchungu ulio kama upanga utachoma moyo wako hakusimama. Maria hakujua mateso yaliyomsubiri kwa kuamua kuwa mama wa Yesu. Tunasali “ Salamu Maria Umejaa Neema.” Alichomwa upanga wa uchungu moyoni.“Salamu Maria Umejaa Neema.” Alikimbilia Misri kumwepusha mtoto Yesu na operesheni ya kamatakamata na chinja watoto iliyoendeshwa na mfalme Herode.“Salamu Maria Umejaa Neema.” Mama Maria alimtafuta mtoto wake amepotea siku tatu. “Salamu Maria Umejaa Neema.” Alikutana na mwanae njia ya kwenda Kalvari (Mahali pa kutundikia watu msalabani). Tunasali “ Salamu Maria Umejaa Neema.” Alisimama chini ya msalaba masaa matatu. Yesu aliposema, “Naona kiu.” Hakuwa na maji ya kumunywesha mwanae. Tunasali “ Salamu Maria Umejaa Neema.” Alikumbatia maiti ya mwanae. Tunasali “Salamu Maria Umejaa Neema.”Alimzika mtoto wake. Penye neema kuna mateso.
Maneno “saa ile ile” yanatupa fundisho pia. Bikira Maria alipoambiwa maneno ya kumchoma moyo kama upanga saa ile ile alifika Anna binti Fanueli wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana. Aliishi na mme wake miaka saba tu. Kisha alikuwa mjane mpaka kufikia umri wa miaka themanini na minne. SAA ILE ILE alifika kumliwaza Bikira Maria labda kumwambia yana mwisho. Kweli penye mateso kuna neema. Unapopatwa na mateso Mungu atatuma neema SAA ILE ILE. Tazama uone neema ya Mungu. Tumuige Anna binti Fanueli anayeenda hekaluni kusali na kufunga.
SALA: Ee Bwana sijui inipasavyo kutoka kanisani wala kuingi. Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima. Amina.