FEBRUARI 1, 2020. JUMAMOSI: JUMA LA 3 LA MWAKA

Mt. Birgida, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: 2 Sam. 12: 1-7, 10-17
Bwana alimtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, “Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au moja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia.” Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, “Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.” Basi, Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe mtu huyo.” Basi, sasa, upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. Bwana asema hivi, “angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Waisraeli wote na mbele ya jua.” Daudi akamwambia Nathani, “Nimemfanyia Bwana dhambi.” Nathani akamwambia Daudi, “Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.” Naye Nathani akatoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51: 10-15 K: Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

  1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, Wala roho yako takatifu usiniondolee.
  2. Unirudishie furaha ya wokovu wako, Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye haki watarejea kwako. (K)
  3. Ee Mungu, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaimba haki yako. Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

INJILI: Mk 4:35-41
Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawaambia, “Na tuvuke mpaka ng’ambo.” Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, “Nyamaza, utulie.” Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, “Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, “Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?”

TAFAKARI:
MUNGU WETU ANAWEZA YOTE: Leo tunajifunza kuwa Mungu wetu anaweza kila jambo. Yaani, hata yale ambayo kwa hali ya kawaida tunaona hayawezekani. Endapo unateswa na ndugu yako kwa muda mrefu au kufanyiwa ukatili wa aina fulani na mtu unayemfahamu, huwa ni vigumu sana kwetu sisi kusamehe. Hili linaoneshwa wazi katika somo la kwanza pale Mfalme Daudi anapoingia tamaa, mbali na kuwa na wake wengi, anamnyang’anya Uria mke wake. Lakini Nabii Nathani anamuonesha mfalme kuwa Mungu hutusamehe makosa yetu tukitubu kwa dhati (Nathani akamwambia Daudi, “Bwana ameiondoa dhambi yako hutakufa.” (2Sam 12:13). Na makuu zaidi yanaonyeshwa na Bwana Yesu Kristo katika Injili anapotuliza dhoruba ya upepo na mawimbi, jambo linalowashangaza wanafunzi wake. Hata sisi tukiwa katika magumu tunayoona hayawezekani, tuyapeleke kwa Mungu naye atatusaidia kwani yeye anatujua zaidi kuliko sisi wenyewe. Tusikate tamaa bali tumtegee yeye kama kimbilio letu hasa nyakati za shida na taabu.

SALA: Ee Bwana, tujalie moyo wa toba ili tuangukapo katika dhambi tuwe na ari na bidii ya kujipatanisha na wewe Bwana Mungu wetu.