Mt. Yohane Bosko, Padre
Kumbukumbu,
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: 2 Sam. 11: 1-10, 13-17
Ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakawahusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, ni mja-mzito. Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, unipelekee Uria, Mhiti, naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa Bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake. Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake. Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe, akafe. Ikawa Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:1-5, 8-9
- Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako;
Kiasi cha wingi wa rehema zako
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Uturehemu, Ee Mungu, kwani tumekosa. - Maana nimejua mimi makosa yangu,
na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho. (K) - Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo
Na kuwa safi utoapo hukumu.
Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu,
Mama yangu alinichukua mimba hatiyani. (K) - Unifanye kusikia furaha na shangwe,
Mifupa uliyoiponda ifurahi.
Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
Uzifute hatiya zangu zote. (K)
INJILI: Mk 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara hupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
TAFAKARI YA LEO:
MCHAKATO WA UFALME WA MBINGUNI:
Katika Injili ya leo Yesu amegusa mambo yanayogusa maisha yetu ya kila siku. Mbegu inaposiwa mpaka itoe mazao ni mchakato wa pekee ambao hata anayesia hiyo mbegu hajui. Mkulima anachojua ni kusubiri mchakato umalizike avune. Ufalme wa mbinguni unafanana na mchakato huo wa mbegu kwani zipo hatua za ufalme huo kukua. Kama mbegu ya haradali ilivyo ndogo ndivyo ufalme wa Mungu unavyoanza, unakuwa na kutawanya matawi yake. Tukuze ufalme wa Mungu kwa kusaidia kukua kwa imani ya wale tunaoishi nao, mfano kufundisha watoto kusali, kusoma Neno la Mungu, kuishi fadhila za kimungu, kusameheana tunapokoseana. Mfano wa mbegu ya haradali ni njia ya kutupa moyo kwa wakristu wanaoishi kwa uchache eneo fulani, labda wakizungukwa na maadui wa imani yao. Watu aliowahubiria Yesu wangeweza kuja duniani leo wangeona jinsi ile mbegu ya Ukristu iliyosiwa wakati wao sasa imekua kubwa na kuenea duniani kote.
SALA: Ee Yesu, nifanye chombo cha kueneza ufalme wako kwa mataifa yote.