JANUARI 30, 2020 ALHAMISI: JUMA LA 3 LA MWAKA

Mt. Yasinta, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: 2 Sam. 7: 18-19. 24-29
Daudi, mfalme, aliingia, akaketi mbele za Bwana, akasema, Mimi ni nani, Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana Mungu. Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee Bwana Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kusema Bwana wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii. Na sasa Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; basi, Sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu, umelinena; na kwa Baraka yako, nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 132. 1-5; 11-14

  1. Bwana, umkumbuke Daudi
    Na taabu zake zote alizotaabika.
    Ndiye aliyemwapia Bwana,
    Akaweka nadhiri kwa shujaa wa Yakobo.
    (K) Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi,
    Baba yake.
  2. Sitaingia hemani mwa nyumba yangu,
    Wala sitapanda matandiko ya kitanda changu;
    Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi
    Wala kope zangu kusinzia,
    Hata nitakapompatia Bwana mahali,
    Na Shujaa wa Yakobo maskani. (K)
  3. Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
    Hatarudi nyuma akalihalifu,
    Baadhi ya wazao wa mwili wako
    Nitawaweka katika kiti chako cha enzi. (K)
  4. Wanao wakiyashika maagano yangu,
    Na shuhuda nitakazowafundisha,
    Watoto wao nao wataketi
    Katika kiti chako cha enzi milele. (K)
  5. Kwakuwa Bwana ameichagua Sayuni,
    Ameitamani akae ndani yake.
    Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
    Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)

INJILI: Mk. 4:21-25
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

TAFAKARI YA LEO:
MAISHA YA MKRISTU NI MWANGA:

Leo katika Injili tumesikia umuhimu wa taa na mahali pake. Neno la Mungu ni taa ambayo inapaswa kuwatoa watu gizani kwa kuwapa nuru. Likibaki likiwa limefungwa tu kwenye Biblia ni sawa na taa iliyowashwa na kuwekwa uvunguni. Likigusa Maisha ya mtu na jamii na hivyo kuleta mabadiliko hapo ni sawa na taa iliyowekwa juu ya kiango. Ni vizuri kujiuliza Neno la Mungu lina nafasi gani katika ratiba yangu. Haitoshi kwenda kusoma Biblia kanisani wakati wa kusikiliza Neno la Mungu, bali Neno hilo lisaidie kukua zaidi kiroho na kuangaza Maisha yetu na ya wenzetu. Tukitaka kupata Baraka za pekee, maadili ya kiroho yanatutaka tusali kwanza. Baadhi ya watu hulalamika na kumlalamikia Mungu kwa kutopata jambo fulani waliloomba. Swali muhimu la kujiuliza ni kuwa tunapoomba au kulalamika, sisi tumetoa kwa namna gani? Tukiwa wakarimu kwa Mungu na kwa wenzetu, Mungu atatutendea kwa ukarimu pia.

SALA: Ee Mungu, naomba Neno lako liangaze Maisha yangu na ya wenzangu.