Mt. Toma wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: 2 Sam. 6:12-15, 17-19
Daudi alienda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng’ombe na kinono. Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la Bwana kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta. wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabariki watu kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 24:7-10
- Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inueni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu?
Ndiye Bwana, Mfalme wa utukufu. - Ni nani mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu hodari,
Bwana hodari wa vita. (K) - Inueni vichwa, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K) - Ni nani huyu wa utukufu?
Bwana wa majeshi, Yeye ndiye mfalme wa utukufu. (K)
INJILI: Mk. 3:31-35
Walikuja mamaye na nduguze wa Yesu; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
TAFAKARI YA LEO:
YESU HAMILIKIWI NI WA WOTE:
Tumesikia katika Injili kuwa Yesu ametembelewa na ndugu zake. Yawezekana walitoka kijijini kwake Nazareti. Kwa hali ya kibinadamu tungedhani kuwa Yesu angeomba udhuru ili awaendee kwanza wageni wake. Badala yake anatumia fursa hiyo kutoa katekesi kuwa watu wote wanaolisikia Neno la Mungu na kulifuata, hao ndio mama yake na ndugu zake. Yesu anatufundisha kuwa familia hazipaswi kuwa sababu ya kusimamisha kazi ya Mungu. Kwa ubatizo wetu sote tumefanywa waana katika familia ya Mungu na Yesu ni ndugu yetu. Tuwaombee viongozi wetu wa Kanisa ili waweze kuwajali wote wanaowaongoza kwa usawa bila upendeleo wowote. Tuziombee pia familia zenye mwelekeo wa kutaka upendeleo wa pekee kutoka kwa viongozi wetu wa Kanisa waache na watambue viongozi hawa wanasimama mahali pa Yesu ambaye hana ubaguzi.
SALA: Ee Yesu, naomba unipe moyo wa kumpokea na kuishi Neno lako daima.