2020 JANUARI 1 JUMATANO: OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

MARIA MTAKATIFU MAMA WA MUNGU
Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO I: Hes. 6:22-27
Bwana alinena na Musa, na kumwambia, “Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; Bwana akubarikie, na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 67:1-2, 4, 6-7

 1. Mungu na atufadhili na kutubariki, Na kutuangazia uso wake.
  Njia yake ijulike duniani, Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
  (K) Mungu na atufadhili na kutubariki.
 2. Mataifa na washangilie, Naam, waimbe kwa furaha,
  Maana kwa haki utawahukumu watu, Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
 3. Nchi imetoa mazao yake; Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
  Mungu atatubariki sisi; Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

SOMO 2: Gal. 4 :4-7
Ndugu zangu: ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

INJILI: LK. 2:16-21
Siku ile: Wachungaji walienda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

TAFAKARI:
THAMANI YA MWANAMKE KATIKA UHAI WA ROHO NA MWILI:

Mwanamke katika utaratibu wa uumbaji Mungu alimpa uwezo wa kuleta mtu duniani kupitia kwa mwili wake. Kumleta kunaambatana na uchungu mkali wa kuzaa ambao pia unaambatana na furaha ya kumleta mtu duniani (Yoh 16:21). Kwa tendo la kukubali kubeba mimba, uhai mpya unaanza. Huyu mwanamke aliyepewa jukumu zito hivyo ndiye aliyeleta pia dhambi duniani baada ya kudanganywa na Ibilisi, lakini kwa huruma, Mungu aliahidi kumtumia aliyezaliwa na mwanamke kumwangamiza Ibilisi (Mwa 3:15). Ndiyo maana, ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, awakomboe waliokuwa chini ya sheria wapate kuwa wana wa Mungu. Ndiyo maana kuzaliwa kwake Yesu kulileta furaha kwa watu wa mataifa mbalimbali hata wakawa na mahangaiko ya kutaka kukutana naye. Huyu ambaye wachungaji walikutana naye, ndiye Mwokozi na furaha ya watu. Mungu alimtumia Mama Maria kutimiza ahadi yake kwa vile alikuwa mwaminifu na kuishi kuandamana na sheria za Mungu.

SALA: Ee Mungu wajalie akina mama watambue nafasi yao katika kazi ya ukombozi.